
KWA mara nyingine, staa anayekimbiza kwenye filamu na muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ au ‘Shishi’ ameibuka katika penzi jipya na bwana mdogo anayechipukia katika muziki wa Bongo Fleva, Nouh Mziwanda, Risasi Mchanganyiko limeinasa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Shilole kwa sasa hasikii wala haoni kwa Nouh pamoja na kwamba wawili hao wanaonekana kuwa na tofauti kubwa ya kiumri , Shilole akionekana kuwa mkubwa zaidi ya Nouh.

Waandishi wetu waliwafuatilia wawili hao kwa nyakati tofauti na kufanikiwa kuzinasa picha zao walizozipiga katika mikao ya kimahaba.
Baada ya kuzinasa picha hizo, mapaparazi wetu walimtafuta Nouh na kumweka mtu kati kuhusu uhusiano wake na Shilole.

Kuhusu tofauti ya umri wake na ule wa Shilole, Nouh alisema umri huwa haumati katika mapenzi.

Pia, Nouh alisema hakutarajia kukubaliwa na Shilole baada ya kumtokea walipokutana katika studio moja jijni Dar na sasa wamekolea kwenye penzi motomoto.

Hata hivyo, Shilole alipozungumza na waandishi wetu alipatwa na kigugumizi kukubali uhusiano wake wa kimapenzi na kinda huyo wa Bongo Fleva.
Shilole alisema Nouh ni rafiki yake kama walivyo marafiki zake wengine.
Waandishi wetu walipomuonesha picha zao walizokuwa wamekaa katika mikao ya kihasarahasara, Shilole aliangua kicheko na kisha akasema:

“Mh! Sina la kuwajibu kama picha zinasema mimi na Nouh ni wapenzi haya.”
Hii siyo mara ya kwanza kwa Shilole kuripotiwa kutoka na Serengeti Boy, siku za nyuma alishawahi kuripotiwa na gazeti dada na hili la Ijumaa Wikienda akisema anapenda kutoka na ‘Serengeti Boys’.